Elimu ya Lishe

LISHE

MLO KAMILI

Mlo kamili ni ule wenye mchanganyiko wa makundi yote ya chakula katika kiwango sahihi kwa ajili ya kuupa mwili nguvu, kuurutubisha kwa ukuaji bora na kuupa kinga dhidi ya magonjwa. Uelewa kuhusu makundi ya chakula na kazi zake utakusaidia kupanga mlo kamili hata kwa gharama kidogo

MAKUNDI YA CHAKULA

i.        Nafaka, Mizizi na Ndizi: Kundi hili ni chanzo kikuu cha nishati mwilini kwani huchngia takribani asilimia 65 ya nishati-mwili kwa siku.

ii.             Mafuta na Sukari: Hili ni kundi linalotoa nishati-mwili kwa wingi. Vyakula vilivyo kwenye kundi hili ni pamoja na asali, sukari/muwa, tende, nazi, samli/jibini na mafuta ya mimea. Mafuta na sukari huupa mwili nguvu na joto. Kwa kawaida mafuta na sukari yanatakiwa yatumike kidogo tu.

iii.            Asili ya wanyama, Maharage na Jamii ya Kunde: Kundi hili ni maalum kwa ajili ya kujenga mwili na kurekebisha sehemu za mwili zilizojeruhiwa au kuzeeka. Kitaalam kundi hili linaitwa Protini. Mfano wa vyanzo vya Protini kutoka kwa wanyama ni; nyama, samaki, kuku na maziwa. Aidha, maharage na jamii ya kunde kwa ujumla ni chanzo kizuri cha Protini kutoka vyanzo vya mimea.

iv.           Matunda: Kazi kuu ya matunda ni kulinda mwili dhidi ya maradhi na kuusaidia kufanya kazi zake za kibaiolojia vizuri.

v.            Mboga: Kazi kuu za mboga ni kulinda mwili dhidi ya maradhi na kuusaidia kufanya kazi zake za kibaiolojia vizuri.

MAMBO YA KUZINGATIA KILA SIKU KUHUSU ULAJI

•             Kula angalau milo mitatu mikuu kwa siku pamoja na asusa (milo midogo) zenye afya kati ya milo mikuu

•             Kula mlo kamili kutoka kwenye makundi yote ya chakula

•             Punguza matumizi ya sukari na vinywaji vyenye sukari. Badala yake pendelea kula nafaka isiyokobolewa na mboga kwenye kila mlo

•             Dhibiti matumizi ya mafuta, pendelea mafuta yasiyoganda kama vile mafuta ya alizeti, mafuta ya mahindi na mafuta ya samaki. Epuka au punguza mafuta ya wanyama

•             Punguza ulaji wa nyama nyekundu, badala yake pendelea kula samaki, maharage na jamii ya kunde.

•             Iwapo una uzito uliozidi wastani wa kiafya, unashauriwa kuondoa ngozi ya nyama ya kuku, kula nyama zisizo na mafuta na kutumia maziwa yaliyopunguzwa mafuta

•             Unaweza kujitahidi kulinganisha mlo wako na kielelezo kilichooneshwa hapa chini ili kujiweka sehemu salama zaidi dhidi ya Magonjwa Sugu yatokanayo na Lishe (MS-L).

MTINDO BORA WA MAISHA

Ili kukabiliana vyema na MS-L, ulaji bora wa chakula ni lazima uambatane na mtindo bora wa maisha ambao unasisitiza; kufanya mazoezi kila siku, kupumzika vya kutosha na kuepuka / kupunguza matumizi ya sigara na pombe.

KUMBUKA

Ulaji wa mlo kamili ni muhimu zaidi katika kuzuia na kutibu Utapiamlo kwa wanawake wajawazito / wanaonyonyesha na watoto ambao mara nyingi ndio wahanga wakubwa wa tatizo hili.